KARIBU KATIKA BLOG YAKO, UNARUHUSIWA KUTOA MAWAZO YAKO YATAKAYOJENGA

MUUNGANO

bofya hapa kudownload historia ya muungano

MUUNGANO kati ya Tanganyika na Zanzibar ndio uliozaa nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo muungano huo ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Karume, umekuwa ukihojiwa mara kwa mara kutokana na kasoro nyingi zilizomo.
Baadhi ya Wazanzibari wamezibainisha kasoro zilizomo kwenye muungano huo na kushauri kufanyika kwa tathmini ya muungano uliopo.
Mkataba wa Zanzibar katika muungano uko wapi?
Kundi la Wazanzibari 15 maarufu kama G15 ni kati ya makundi mbalimbali vinavyojitokeza kuhoji uhalali wa muungano huku vingine vikishia kuishitaki serikali mahakamani.
Kundi hilo limejitokeza tangu mwaka 2005 ambapo liliishitaki Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kupata mkataba huo. Ndipo ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Zanzibar ilipokiri kutokuwa na mkataba huo.
Mwaka 2010 kundi hilo liliandika barua Umoja wa Mataifa kutaka muungano huo ufanyiwe tathmini upya.
Mbali na Umoja wa Mataifa, wamepeleka nakala ya barua hiyo katika balozi za nchi za Marekani, Uingereza, Urusi, Ufaransa, Ujerumani na Umoja wa Nchi huru za Afrika.
Makamu mwenyekiti wa G 15, Rashid Yusuf Mshenga anasema kuwa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar haukuwa na uhalali kwakuwa Zanzibar hawakupewa mkataba.

“Muungano huu ni ‘verbal’ tu, ni wa kuchanganya mchanga tu wan chi mbili, lakini ukiuliza Mkataba wa muungano haupo. Tunataka muuungano huu upitiwe upya,” anasema Mshenga.
Anasema kuwa upande wa Tanzania bara walipata mkataba wa Muungano uliokuwa umesainiwa, lakini upande wa Zanzibar mkataba huo haukupatikana hali inayotia shaka katika muungano,
“Wenzetu bara, Spika wa kwanza Adam Sapi Mkwawa na Pius Msekwa walibaki na nakala ya Mkataba, lakini Zanzibar hadi leo haupo, wala hakukuwa na Barza la Mapinduzi lililokaa kujadili muungano. Hata Mzee Aboud Jumbe alipoingia madarakani alikiri kuwa hakukuwa na  mkataba” anasema.

Mshenga ameshangazwa na Serikali ya Muungano na SMZ kuweka kamati ya kushughulikia kero za Muungano wakati hata Mkataba wa muungano haupo akisema kuwa hiyo ndiyo kero ya kwanza.
“Kamati ya kushughulikia kero za muungano inaundwa na makada wa CCM, kama Waziri mkuu na viongozi wa SMZ, wote hawawezi kuhoji mambo muhimu”.
Mshenga ameshauri kuwa ili kupata uhalali wa Muungano, Serikali ya Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waunde timu za kuujadili muungano kasha iitishwe kura ya maoni ili wananchi waamue muungano wanaoutaka.

Kwa upande wake Nassor Hassan Moyo aambaye ni mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na muungano huo, ameshangazwa na madai kuwa Zanzibar haikupata mkataba.
Anasema mkataba ni moja kati ya nyaraka muhimu za serikali hivyo wanaopaswa kuwajibika ni Ikulu ya Zanzibar na ofisi ya Mwanasheria.
Akieleza jinsi hatua za kuunganisha Tanganyika na Zanzibar zilivyofikiwa, Moyo anasema kuwa muungano ulifanywa na kiurafiki zaidi.
“Wakati ule Mwalimu Nyerere na Karume walikutana kukubaliana kuungana. Baada ya makubaliano hayo, Mwalimu na ujumbe wake wakiwamo Oscar Kambona, Bokhe Munankha, Job Lusinde na Ali Mwinyi Tambwe walikuja Zanzibar na kusaini mkataba wa muungano. Kwa upande wa Zanzibar walikuwapo Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo.
Baada ya hapo Karume aliitisha Baraza la Mapinduzi na kutueleza. Tulimuuliza baadhi ya mambo kama vile elimu ya bure, afya kama bado vitatolewa bure, akasema vitaendelea hivyo na sisi tukaafiki” anasema Moyo.
Lakini Moyo anasema kuwa kwa wakati ule hakukuwa na mwamko mkubwa wa watu kuhoji mambo tofauti na sasa.
“Naunga mkono vijana wanaohoji muungano, muungano ni wao, sisi muda wetu umekwisha, wananchi wanahaki ya kuhoji uhalali wa muungano.” anasema Moyo.
Huku akionyesha kuguswa na ibara ya 9(2) ya muswada wa marejeo ya Katiba inayokataza wananchi kuyaondoa mambo muhimu kama vile muungano, urais, uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mengineyo, Moyo alisema kuwa wananchi wasizuiwe kuyajadili mambo hayo.

“Kwa sasa serikali inafanya jitihada za kurekebisha Katiba ambapo pia muungano utaangaliwa. Lakini sasa wamezuia mambo muhimu kuzungumziwa. Kwanini uwazuie watu kujadili muungano, kwanini wanasiasa wasishiriki kwenye mchakato wa Katiba? Nyerere hakuwa askofu wala Karume hakuwa mufti, wote walikuwa wanasiasa na ndiyo waliounda muungano, kwanini wanasiasa wa leo wasiruhusiwe?” anasema Moyo.
Maswali mengi bila majibu
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, anasema muungano una kasoro za msingi za kimaumbile.
Anazibainisha kasoro hizo ambazo anasema ni miongoni mwa sababu za muungano kuwa na kero sugu kuwa ni  kuwepo kwa masuala ya msingi ya kikatiba ambayo hayana majibu ama kutoka ndani ya Katiba, Sheria, Sera na hata kutoka kwa watendaji.
Utata wa kwanza kwa mujibu wa Othman ni kama washiriki wa muungano bado wapo au hawapo?
“Kwa vile nchi ambazo zimeungana kwa baadhi ya mambo tu, inategemewa kwamba waliounganisha mambo hayo wapo, wana vikao rasmi vinavyotambuliwa na Katiba na Sheria za Nchi. 
Ilitegemea kuwa Washirika hao wanaamua kuongeza kupunguza mambo ya Muungano wakiwa na nguvu sawa ya uamuzi.  Ilitegemea kuwa Washirika hao wana kauli sawa za maamuzi juu sera, uendeshaji na Sheria za Muungano.  Suala ni kuwa hivi ndivyo hali ilivyo?” anahoji.

Kuhusu mambo ya muungano, Othman anajadili maana ya mambo ya muungano na idadi yake.

Anafafanua kuwa,  jambo linapoitwa la Muungano ni kuwa Zanzibar haina uwezo wa kulisimamia kisera, kiutawala na kisheria.
“Hata hivyo suala hili ni gumu kuliko linavyoonekana.   Kabla ya kuja sera za biashara Huria mashirika kama vile Air Tanzania, Shirika la Posta na Simu na Benki ya Taifa ya Biashara na mengineyo yakijulikana kama mashirika ya Muungano.  Katika vikao kadhaa ilikubaliwa kuwa Zanzibar ishirikishwe katika uendeshaji wa mashirika hayo ya Muungano. Mashirika hayo mengi yamebinafsishwa” anasema Othman.

Kuhusu uwakilishi wa Zanzibar katika muungano
kupitia Rais wa Zanzibar ambaye alikuwa Makamo wa Rais wa Muungano kwa kupitia wadhifa wake wa Urais wa Zanzibar, Othman anajadili marekeisho ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya muungano,

“Baada ya Marekebisho ya 11 ya Katiba Rais wa Zanzibar aliondolewa katika nafasi ya Makamo wa Rais kwa kupitia wadhifa wake.  Badala yake Makamo wa Rais anapatikana na utaratibu wa Mgombea Mwenza.  Chini ya ibara ya 47(3) ya Katiba ya Muungano, Mgombea Mwenza anateuliwa kwa Kanuni kuwa iwapo Rais ni mtu anayetoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Makamo wa Rais awe ni mtu anayetoka upande wa pili wa Muungano”.

Kuhusu Uchumi, Othman ananukuu Kitabu cha Muafaka baina ya SMT na SMZ kinachoeleza kuwa “Tanzania ni nchi moja yenye uchumi mmoja wenye mazingira tofauti”, lakini anasema katika utekelezaji Serikali zote mbili zinaonyesha kuwa na jibu tofauti – kwamba uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar ni tofauti.
“Mtafaruku uliopo unatokana na ukweli kwamba ingawa chumi ni mbili lakini nyenzo zote kuu za uchumi zinadhibitiwa na Serikali ya Muungano.  Nyenzo kama vile udhibiti wa sera za fedha, kodi na mahusiano na nchi za nje hazimo mikononi mwa Zanzibar ingawa Zanzibar inategemea ijiendeshe kiuchumi”.
Nini kifanyike?

Ili kuudumisha muungano, Othman anasema kuwa hautalindwa kwa siasa na kuusifu pekee na kuwaita wale wanaoukosoa kuwa ni maadui wa Muungano ingawa wapenzi wa Muungano wenyewe wanazikubali kasoro hizo hizo na hata wameziandika na kuzifanyia vikao. 

“Muungano utalindwa kwa kuwekewa misingi madhubuti iliyo wazi na ambayo italindwa kwa misingi ya Katiba na Sheria inayokubalika na ambayo itatokana na ridhaa za washirika wa Muungano”.

Akitoa mfano wa Uingereza na Scotland, Othman anasema kuwa kumekuwa na marekebisho kadhaa ya kuboresha muungano wao, tofauti katika Muungano wa Tanzania ambapo marekebisho mengi ya kikatiba, kishera na kisera yanafanya Muungano kuwa na matatizo zaidi kwa vile kiini cha Kero za Muungano hakijashughulikiwa.  Maswali ambayo hayana majibu ni mengi ndani ya Muungano.

“Hakuna Muungano madhubuti ambao unategemea kulindwa na sera za chama.  Muungano madhubuti ni ule unaolindwa na misingi madhubuti, uwazi na wenye majibu kwa masuali yanayohusu nguzo kuu za Muungano huo,” anasema Othman.

0 comments:

Html Free Code

wibiya widget